Mpenzi msomaji wangu, kila unapofanya kosa kuna maswali mwenzi wako huwa anajiuliza.
Hayo maswali baadae ndiyo hutoa jibu litakalofanya akuone kama wewe si mtu mwafaka kwake.
Kinachotafutwa katika mapenzi si kuwa na mtu mwenye sura nzuri sana au kuwa na mtu mahiri sana kitandani pekee, hapana.
Japo hayo ni mambo yana maana yake katika namna yake ila muhimu zaidi ni kuwa na mtu anayeweza kumsababishia furaha mwenzake.
Katika huzuni awe na uwezo wa kumfanya mhusika akatabasamu. Katika majonzi kuwe na hali ya unafuu na maisha kutoa maana chanya.
Kama kila siku katika uhusiano ni makosa ya kujirudia ni kwa namna gani atakufikiria kama mtu mwafaka kwake?
Fikra zake ni lazima ziondoke katika kukufikiria kama mtu bora kwake na badala yake akuone mtu usiyefaa wala wa thamani katika maisha yake.
Japo huwa anasema anakusamehe ila kumbukumbu ya kosa lako huwa linabaki katika ubongo. Unaweza kufanya akaendelea kukuona bora kwa kufanya matendo bora na ya maana katika maisha yake.
Au unaweza kumfanya akakuona si lolote kwa kila siku kurudia yale ambayo unajua yanamsababishia simanzi na unyonge.
Nimeshawahi kusema kuwa, katika uhusiano hakuna kosa dogo. Kama kitendo chako kinamtoa katika hali ya amani na furaha, hakijalishi kiko namna gani basi kichukulie kuwa ni kosa kubwa.
Msamaha huwa unafuta kosa katika meza ya majadiliano ila huwa hauondoi kumbukumbu nzima ya kosa. Kuwa makini na matendo yako.
Suala si kusamehewa, ila ni kwanini kila siku unakosea wewe? Kuwapo kwa msamaha si ruhusa ya kukoseana.
Mapenzi ni suala la hisia. Kama ukiweza kufanya kila siku akahisi amani na furaha ina maana atakuona mpenzi bora na kama utamfanya ajihisi mnyonge na kumpa mashaka, atakuona mpenzi usiyefaa. Kuwa makini.
Kama kweli unamhitaji katika maisha yako, mfanye awe na furaha.
Epuka kumkosea na jitahidi kumfanya ajione kuwa kapata mtu sahihi na mwafaka katika maisha yake.
Kwa hayo machache naona nifikie hapa, bila shaka umejifunza kitu hapa.
Tukutane kesho panapo majaaliwa .
Comments
Post a Comment